TANGAZO MAALUM

TANGAZO MAALUM
.

TANGAZA NA SISI

TANGAZA NA SISI KWA BEI NAFUU TUPIGIE KUPITIA 0713 57 57 18 AU TUMA BARUA PEPE DTV@EML.CO.TZ

Monday, August 26, 2013

VITA YA MADAWA YA KULEVYA YAZIDI KUPASUA, VIONGOZI WOTE WA SERIKALI KUKAGULIWA UWANJA WA NDEGE ISIPOKUWA WATANO "5" TU!



  Na Mwandishi Wetu
KUANZIA sasa viongozi wote serikalini watakaopita kwenye viwanja vya ndege nchini, watakuwa wakikaguliwa kama abiria wengine, isipokuwa Rais, Makamu wake, Waziri Mkuu, Jaji Mkuu na Spika wa Bunge.

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema ipo tabia ya viongozi wenye madaraka, kukiuka utaratibu na kupita katika viwanja vya ndege bila kukaguliwa.

Alisema kutokana na hali hiyo, amewaambia watumishi wanaofanya kazi katika viwanja hivyo, hususan Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) viongozi wasiokaguliwa ni Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Jaji Mkuu na Spika wa Bunge.

Alitoa msimamo huo wiki iliyopita kupitia kipindi cha Jenerali on Monday, kinachorushwa na Televisheni ya Channel Ten. Alisema viongozi wengine wote, wakiwamo mabalozi na mawaziri lazima wakaguliwe.

Dk Mwakyembe alisema aliwaambia viongozi wasiopenda kukaguliwa, wasipande ndege. Alisema pamoja na 
baadhi kuona ni usumbufu, inawezekana wakajikuta wamesahau vitu hatari, kama vile risasi na wakaenda kugundulika nje ya nchi ikawa tatizo.

Alitoa mfano kwamba aliwahi kupigiwa simu na mmoja wa mabalozi, akilalamika kwamba vijana wake wamemkagua uwanja wa ndege.

Alisema alimjibu kwamba wanatimiza wajibu wao. Katika mahojiano yaliyojikita juu ya tatizo la dawa za kulevya nchini, Dk Mwakyembe alisisitiza kwamba hatua alizoanza kuchukua kudhibiti upitishaji dawa hizo kwenye viwanja vya ndege, siyo moto wa kifuu wala nguvu ya soda.

“Ninachokifanya hapa ni kile ambacho kinapaswa kufanywa… na hili la dawa za kulevya katika viwanja vya ndege, nitalikomesha,” alisema. Alisisitiza kwamba udhibiti huo ni kwa viwanja vyote vya ndege nchini. Dk Mwakyembe alisema, “kwa sasa mizigo yote inayoingia katika eneo hilo, lazima ikaguliwe, kwani huo sio mzaha, sio moto wa kifuu wala nguvu ya soda.”

Kwa mujibu wa Waziri, mizigo inayoingia imekuwa haikaguliwi. Alisema katika kutekeleza ukaguzi huo wa mizigo inayoingia, imenunuliwa mitambo kwa ajili hiyo.
 Kuhusu wanaomeza dawa za kulevya, alisema wamekuwa wakigundulika kutokana na ufuatiliaji kuanzia kwenye ndege. Alitoa mfano kwamba kwa sasa endapo abiria atapanda ndege katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, mathalani kwenda Dubai, akipewa chai au pombe, akakataa kunywa, kwa vyovyote huyo lazima akaguliwe zaidi.

Katika hilo, aliwaasa vijana wa Tanzania kujiepusha na hali hiyo, kwani pindi akishuka kwenye uwanja wowote, namba yake ya kiti itashikiliwa na atakaguliwa ipasavyo, kubaini kama amemeza dawa.

Hatua ya Mwakyembe kuamua kuvalia njuga dawa za kulevya, inatokana na kile ambacho kinaelezwa kuwa ni kuchafuka kwa Tanzania, kutokana na baadhi ya watanzania kukamatwa nje ya nchi, wakisafirisha dawa hizo, wakiwa wamezipitisha uwanja wa ndege.

Dk Mwakyembe alieleza kuwa hatua yake ya kuvalia njuga suala hilo, inaungwa mkono na serikali kwa ujumla. Hivi karibuni waziri huyo alifanya ziara ya ghafla katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere na kubaini kuwa tatizo si vifaa vya ukaguzi, bali ni baadhi ya wafanyakazi wasio waadilifu.

Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene alisema hivi karibuni serikali imeanzisha mkakati wa kutokomeza wimbi la dawa za kulevya kwa kudhibiti viwanja vya ndege na sehemu mbalimbali za mipakani, zinazotumiwa kupitisha. ---
 HabariLeo

No comments:

Post a Comment