MKAZI wa Kijiji cha Mlongazila, wilayani Kisarawe, Pwani, Moshi
Hamad anatuhumiwa kumng’ata mwanaye, Khadija Hamad (6) sehemu za siri
kwa madai ya kujisaidia haja kubwa na ndogo hovyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima juzi wilayani
Kisarawe, wakazi hao walisema mama huyo amekuwa na tabia ya kumfungia
ndani mtoto wake huyo na kumchapa kwa zaidi ya nusu saa, akitumia nyaya
za simu na kumng’ata sehemu mbalimbali za mwili zikiwamo za siri na
kumsababishia maumivu makali.
Wakazi hao walisema waliamua kutoa taarifa kwenye dawati la haki za
binadamu baada ya kuchoshwa na vitendo hivyo, na sasa wamelitaka Jeshi
la Polisi kumkamata mama huyo na kumchukulia hatua.
Stella Musa, alisema sehemu za siri za mtoto huyo zimeharibiwa
kutokana na kung’atwa na meno, huku zikiwa na vidonda vinavyodaiwa
vimetokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.
“Wazazi wa mtoto huyo ni wanangu, siku moja mama huyo alimuumiza
mkono. Nilimchukua na kukaa naye nyumbani kwangu kwa mwezi mmoja
nikimuhudumia kwa kumkanda kwa maji ya moto,” alisema Stella.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Mlongazila, Paulo Idana ambaye pia ni
katibu wa dawati la kutetea haki za binadamu, alisema suala hilo
limewafikia, hivyo wanachukua hatua za kisheria huku mtoto huyo amewekwa
chini yao kwa matibabu zaidi.
“Tulimfuata mama huyo Septemba 20 mwaka huu na tulifanya nae mahojiano
mbele ya ofisa mtendaji wa kijiji na alikiri akisema alifanya hivyo kwa
sababu ya hasira. Tunafanya utaratibu ili tumfikishe kwenye vyombo vya
sheria,” alisema Idana.
Akieleza mkasa huo, mtoto huyo alisema wakati mwingine mama yake
alikuwa akimwita ili amfundishe kusoma na aliposhindwa aling’atwa
mgongoni, mapajani na sehemu za siri huku akisema atamfanyia hivyo hadi
ajue kusoma.
Mama wa mtoto huyo, Moshi, alisema alikuwa akitoa adhabu kwa mwanaye
huyo kutokana na kujisaidia haja ndogo na kubwa hovyo wakati akirudi
shule.
“Nafanya hivi kutokana na hasira siwezi nikamuona mtoto wangu
anajisaidia haja kubwa na ndogo kwenye nguo nikamwacha tu, lazima
nimwadhibu… jana alitapika kwenye sahani. Je, mtoto kama huyu
nitamwacha?” alihoji Moshi.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Khadija Samizi alikiri kuwepo kwa tukio hilo.
No comments:
Post a Comment