JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limeleezea namna mwanajeshi wake, Meja Khatibu Shaaban Mshindo, alivyouawa baada ya kuangukiwa na bomu, wakati akiwa katika jukumu la ulinzi wa amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Pamoja
na hayo, Watanzania wametakiwa kuimarisha mshikamano na kuachana na
makundi yenye nia ya kuleta mgawanyiko, hasa katika kipindi hiki kigumu
ambacho Tanzania imepoteza askari wake waliopewa dhamana ya kitaifa ya
ulinzi wa amani katika nchi zenye migogoro Afrika.
Akitoa
salamu za rambirambi wakati askari huyo wa kikosi cha Mizinga namba 83
KJ kilichopo Kibaha akiagwa rasmi kijeshi Dar es Salaam jana, Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamnyange, alisema askari huyo pamoja
na askari watano wa Tanzania, waliangukiwa na bomu hilo na kujeruhiwa
vibaya.
“Waliangukiwa
na bomu Agosti 28, mwaka huu huko Goma DRC eneo walilokuwa wakifanyia
kazi… Meja Mshindo aliumia vibaya na kukutwa na mauti njiani akipelekwa
hospitalini,” alisema Jenerali Mwamunyange.
Alisema
katika tukio hilo, askari wengine watano wa Tanzania walijeruhiwa
vibaya na wanaendelea vizuri na matibabu nchini humo na hali zao
zinaendelea vizuri.
Akimzungumzia
Meja Mshindo, Jenerali Mwamunyange alisema katika uhai wake alikuwa
mchapakazi, muaminifu, hodari na mtiifu na kifo chake kimetokea wakati
jeshi linamhitaji.
“Kifo
chake kimeacha pengo ndani ya JWTZ na itachukua muda mrefu kuziba pengo
hili.” Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, alisema kifo cha askari huyo ni msiba wa kitaifa na kumtaja Meja
Mshindo kuwa shujaa aliyekutwa na mauti wakati akitekeleza kazi
aliyotumwa na nchi yake.
Alisema
kifo hicho pamoja na vifo vya askari wengine saba wa JWTZ vilivyotokea
Darfur mwaka huu, ni chachu kwa Tanzania kuendeleza jitihada za kusaidia
nchi zenye migogoro na kuhamasisha amani Afrika.
“Serikali inapata matumaini namna Watanzania walivyosimama pamoja na kuunga mkono jeshi letu katika kipindi hiki kigumu. Ingekuwa nchi nyingine, haya yaliyotokea yangeleta mgawanyiko mkubwa miongoni mwa raia, lakini kwa hapa kwetu hali imekuwa tofauti,” alisema Membe.
Aliwataka
wachache wenye mawazo ya kutumia matukio hayo kuwagawa Watanzania,
waache mara moja nia yao hiyo, kwa kuwa moja ya kazi ambayo Tanzania
inayo, ni pamoja na nia yake ya kuhamasisha na kutangaza amani Afrika na
dunia kwa ujumla.
“Jamani
wajibu wetu ni kuhakikisha haya maeneo yenye migogoro yanakuwa na
amani, kule DRC hali ni mbaya, watu wanakufa kila kukicha na akinamama
na watoto wanabakwa na kudhalilishwa, sasa sisi kama taifa ni vyema
kujitokeza na kusaidia wenzetu,” alisisitiza.
Meja
mshindo, alizikwa jana nyumbani kwao Fujoni Zanzibar na ameacha mke
mmoja, Hawa Mnimbo na watoto watatu ambao ni Shaaban, Abuu na Samir
Mshindo.
No comments:
Post a Comment