Na Mwandishi wetu
WAKATI kelele za wasanii wa fani zote nchini zikiendelea
kusikika kuhusu wizi na dhuluma bila mkombozi thabiti kuonekana, wasanii
waliopanda jukwaani kuimba siku ya tamasha la waendesha pikipiki jijini Dar es
Salaam ambalo lilihitimishwa kwa hotuba ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
walipunjwa malipo waliyopewa.
Chanzo cha uhakika kilicho karibu na walioratibu, kusimamia
na kushiriki maandalizi ya tamasha hilo, kinasema kigogo mmoja anayelalamikiwa
sana na wana Bongo Fleva kuwa amekuwa akiwadhulumu na kukandamiza haki zao, alipewa
tenda ya kuwatafuta, kuzungumza na hatimaye kuwalipa wasanii watakaoimba siku
hiyo ya tukio lililofanyika katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini
Dar es Salaam m.
Inadaiwa kuwa wakati wa majadiliano ya tenda hiyo, kigogo
huyo alitoa bei kubwa kwa waratibu wa tamasha hilo, akidai wasanii wa siku hizi
wameshtuka na wanataka fedha nyingi, jambo ambalo lilikubaliwa na watayarishaji
hao, waliokuwa chini ya mtoto wa Mheshimiwa Lowassa aitwaye Fredy.
Inadaiwa kigogo huyo alitaja fedha ambazo kila msanii alistahili
kupewa na zikatolewa (Fedha ya chini kabisa inasemekana ilikuwa shilingi
milioni 1), kulingana na hadhi, ubora na kukubalika kwa wasanii hao kwa sasa.
“Baada ya tamasha kukamilika, msanii mmoja alilalamika
kuhusu kiwango kidogo cha fedha alizopata, mmoja wa waamndaaji alipodadisi
kiasi alichopewa, akamwambia laki mbili. Akamwambia ameibiwa, akamshauri aende
kwa Fredy kwa sababu yeye ndiye aliyekuwa akisimamia malipo ya wasanii, alipokwenda
na kumweleza, Fredy alishangaa sana, akamuonyesha jinsi ambayo kila msanii
alipaswa kulipwa,” kilisema chanzo hicho.
Inadaiwa baada ya msanii huyo kuonyeshwa malipo
yaliyotolewa alishangaa sana na alipodai kupewa kilichobaki, aliambiwa aende
kwa kigogo huyo, lakini kutokana na hofu iliyojengwa dhidi ya mtu huyo, msanii
huyo alinywea na kumezea.
“Wasanii wanamuogopa sana jamaa (linatajwa jina la kigogo
huyo), wengi walikwenda kulalamika, lakini wakaambiwa waende wakamweleze kisha
wapeleke majibu kwa Fredy, lakini hakuna aliyekwenda,” kilisema chanzo hicho.
Xdeejayz lilimvutia waya mlalamikiwa, ambaye anatajwa
kuwa karibu na wadau wote wanaojihusisha na muziki Tanzania, kiasi cha
kuonekana kama Mungu mtu miongoni mwa wanamuziki na wasanii.
Simu yake ya kiganjani iliita kwa muda wote bila kupokelewa
hata baada ya kupigiwa zaidi ya mara moja. Kana kwamba haitoshi, gazeti hili
lilituma ujumbe mfupi wa maandishi (sms) likiomba kujibiwa kwa maswali hayo,
lakini bado kigogo aliendelea kuuchuna. Hata hivyo, juhudi za kuwatafuta wadau
zaidi wa sakata hili zinaendelea.
"GAZETI LA MASKANI BONGO LIKO MTAANI KILA JUMATANO DAKA KOPI YAKO"
No comments:
Post a Comment