MAJAMBAZI jana yalifanya onesho la aina yake jijini Dar es Salaam, baada ya kupora mamilioni ya shilingi katika kituo cha mafuta cha Lake Oil, Buguruni Malapa na kumwaga fedha hizo kwa wananchi maeneo ya Tazara ili kuhadaa polisi.
Wakiwa katika pikipiki aina ya Toyo na fuko la fedha, majambazi hao baada ya kupora fedha hizo, walifanikiwa kupita katika foleni ya magari mpaka katika taa za Tazara.
Walipofika katika eneo hilo, ghafla polisi wenye silaha wakiwa katika pikipiki zaidi 10, walivamia na kusababisha majambazi hao kurusha sehemu ya fedha walizo pora hewani.
Shuhuda mmoja wa tukio hilo, anayeuza bidhaa mbalimbali akiwa amebeba mkononi katika eneo la Tazara, alieleza gazeti hili kuwa walijikuta wakikimbilia fedha hizo, kitendo kilichosababisha polisi kushindwa kutambua majambazi hao.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, wakati wananchi wakigombea fedha hizo, huku polisi wakihangaika kutaka kukamata watuhumiwa, majambazi hao walirukia gari aina ya Suzuki Pick Up.
Shuhuda huyo alidai majambazi hao walimwamuru dereva kuondoka, lakini dereva huyo alikumbwa na bumbuwazi, asijue la kufanya. Kutokana na kushindwa kuondoka, papo hapo walimjeruhi kwa risasi.
Muuza CD
Mtu mwingine ambaye alikuwa abiria katika gari hiyo, alipoona wamevamiwa, aliruka na kuanza kutimua mbio kwenda upande wa soko la Vetenari.
Hali hiyo ilisababisha polisi waliokuwa katika eneo hilo wakiwa na pikipiki, kuanza kumfukuza.
Waandishi wetu walishuhudia zaidi ya pikipiki nne za polisi, waliokuwa wakipiga risasi za moto hewani, wakimkimbiza abiria huyo, ambaye baadae alikutwa katika soko la Vetenari, karibu na ukuta wa TBC na aligundulika ni muuzaji wa CD za reja reja.
Baada ya muda mfupi, kundi la Polisi ambalo liliwasili katika eneo la tukio, lilifanikiwa kuwadhibiti majambazi hao, ambao awali walidaiwa kuwa watatu huku mmoja wao akiwa na silaha.
Polisi hao pia walionekana kuchukua fuko hilo la fedha na kuliingiza katika moja ya magari sita, yaliyokuwa na polisi hao. Aidha, watuhumiwa hao walipandishwa katika gari tofauti na lililobeba fedha hizo, huku wakivuja damu.
Gari hilo lilizungukwa na askari wa doria maalumu ya kudhibiti ujambazi jijini Dar es Salaam. Mbali na magari hayo, pia pikipiki za Polisi zilikuwa nyingi, jambo ambalo liliwatia moyo wananchi waliofika katika eneo hilo, kuwashuhudia majambazi hao na wengine walisikika wakisema ‘Polisi leo (jana) wamefanya kazi yao ipasavyo’.
Hata hivyo, wananchi hao walitaka wahalifu hao wasulubiwe papo hapo.
Akizungumzia hili, askari aliyekuwepo katika eneo hilo huku akikataa kutaja jina lake, alisema wamekamata majambazi wawili, ambao walipora fedha katika eneo la Buguruni Malapa na mmoja amekimbia.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema ofisi yake inakamilisha upelelezi, na leo taarifa kamili itatolewa kupitia Kanda Maalumu ya Kipolisi.
No comments:
Post a Comment